Katika Mawasiliano ya Wahudumu wa Bodaboda na Abiria: Uchunguzi Kifani wa Kaunti ndogo ya Mbooni, Makueni, Kenya

Abstract

Bodaboda ni baadhi ya vyombo vya usafiri ambavyo hutumika kote ulimwenguni ili kukidhi utashi wa usafiri kwa wanadamu. Utafiti huu ulijikita katika kuchunguza mikakati ya upole na namna wahudumu wa bodaboda wanaizingatia au kuikiuka wanapoingiliana na wateja wao. Mawasiliano mema huchochea uwezo wa wahudumu wa bodaboda wa kuvutia na kudumisha uhusiano wao na abiria. Ufanisi wa mazungumzo haya hutegemea uwezo wa wanaohusika kutumia mikakati ya upole. Wanajamii hutumia mikakati ya upole ili kujaribu kulinda nyuso zao au za wanaotagusana nao. Utafiti huu ulitathmini mikakati ya upole kama inavyotumika katika mawasiliano baina ya wahudumu wa bodaboda na abiria katika eneo la Mbooni lililo katika Kaunti ya Makueni. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Upole. Usampulishaji ulifanywa kimakusudi ili kupata sampuli ya data iliyokuwa na sifa za kuwezesha ufikiaji wa malengo ya utafiti. Utafiti huu wa kithamano ulihusisha uchunzaji wa mawasiliano 26 kati ya wahudumu wa bodaboda na abiria kisha mahojiano 58 yaliyohusisha wahudumu wa bodaboda 30 na abiria 28 kutoka kwa vituo vitano. Idadi hii ya sampuli ilitokana na ufikiaji wa kiwango kifu kwenye mchakato wa ukusanyaji data. Mbinu za kukusanya data katika utafiti huu zilikuwa ni uchunzaji na mahojiano ya moja kwa moja ambapo mawasiliano yalirekodiwa kwa kutumia kinasa sauti. Mawasiliano yaliyokuwa yamerekodiwa yalisikilizwa na kunakiliwa kwa ajili ya uchambuzi. Uchanganuzi wa data katika lengo la kwanza ulihusisha kuhakiki na kuelezea kwa kina kauli zilizotumika katika mawasiliano ili kubainisha mikakati ya upole kwa kuzingatia mihimili ya nadharia husika. Kwa lengo la pili na la tatu, data kutoka kwa watafitiwa ilihakikiwa na kuelezwa kwa kuelekezwa na nadharia ya upole. Kulingana na matokeo ya lengo la kwanza, mikakati yote ya upole ilitumika katika mawasiliano ya wahudumu wa bodaboda na abiria ila mkakati chanya wa upole, mkakati ndani ya rekodi na mkakati nje ya rekodi ulitumika kwa wingi. Mkakati hasi na wa kutosema chochote ulitumika kwa kiwango cha chini. Lengo la pili lilidhihirisha kuwa, ili kuzingatia matumizi ya mikakati ya upole wahudumu wa bodaboda na abiria huchochewa na faida au matokeo tarajiwa, tofauti za mahusiano kama vile ya umri, haja ya kutaka kuonyesha heshima kwa sababu ya tofauti za kimamlaka na hali ya kutaka kukabiliana na uzito wa tendo la kutishia uso. Hata hivyo, matumizi ya mikakati ya upole hukiukwa kwa sababu ya machukulio, madharau na haraka. Matokeo katika lengo la tatu yalidhihirisha kuwa, matumizi ya mikakati ya upole huwa na athari chanya kwa mawasiliano kama vile; kudumisha heshima, kuleta athari ya raghba, kuokoa muda, kufanikisha mawasiliano, kupoza hisia za hasira na kujenga mahusiano thabiti kati ya wahudumu wa bodaboda na abiria. Kwa upande mwingine, ukiukaji wa matumizi ya mikakati ya upole ulidhihirisha athari hasi kwa mawasiliano kama vile kuzungumzia mada nyeti hadharani na kusitisha mawasiliano baada ya nyuso kutishiwa. Matokeo haya yanaonyesha umuhimu wa mikakati ya upole katika kuboresha mawasiliano ya wahudumu wa bodaboda na abiria. Utafiti huu unawapendekezea watunga sera katika sekta ya bodaboda wabuni na watekeleze sera zinazolenga kuhimiza matumizi ya lugha ya upole kama mkakati wa kuboresha uzoefu na hali ya kuridhika kwa abiria. Vilevile, utafiti huu unatoa mchango muhimu katika taaluma ya Isimujamii na Pragmatiki, hivyo ni wenzo muhimu kwa tafiti za baadaye.

Description

Keywords

Citation