Usawiri wa Mwanasiasa wa Afrika Katika Ushairi wa Kiswahili
Abstract
Utafiti huu ulishughulikia usawiri wa mwanasiasa wa Afrika katika ushairi wa
Kiswahili. Kimsingi, mtafiti alichunguza jinsi washairi mbalimbali walivyowasawiri
wanasiasa wa Afrika kiubunifu kwa lengo la kudhihirisha walivyobadilika kisiasa na
kimaadili kutoka enzi za ukoloni hadi kipindi cha siasa za vyama vingi. Utafiti huu
ulichukulia kuwa wanasiasa hawa hutekeleza wajibu mkubwa katika maendeleo ya
mataifa yao na bara la Afrika kwa jumla. Uafikiaji wa malengo mbalimbali ya
maendeleo kama vile Ruwaza ya 2030 nchini Kenya na uimarishaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa kiasi kikubwa utategemea maamuzi ya kisiasa. Madhumuni ya
utafiti huu yalikuwa kuchunguza nafasi ya ushairi wa Kiswahili katika uhifadhi wa
historia ya mwanasiasa wa Afrika; kubainisha sifa za mwanasiasa wa Afrika kabla ya
uhuru na kutathmini mabadiliko ya mwanasiasa wa Afrika baada ya uhuru kwa
mujibu wa washairi wa Kiswahili. Mtafiti aliichukulia sauti ya mshairi kuwa sauti ya
mwananchi ambaye ndiye huathiriwa na maamuzi na vitendo vya wanasiasa. Utafiti
huu uliongozwa na Nadharia ya Ulimbwende iliyoasisiwa na William Wordsworth na
Samuel Taylor Coleridge na Nadharia ya Baada-Ukoloni ambayo inahusishwa na kazi
za Edward W. Said, Gayatri Chakravorty Spivak na Homi K. Bhabha. Utafiti huu
ulifanyiwa maktabani ambapo mbinu ya sampuli ya kudhamiria ilitumiwa kuteua data
kutoka kwa diwani teule. Uchanganuzi wa kimaelezo ulizingatiwa ambapo mashairi
yaliyoteuliwa yalihakikiwa kwa mujibu wa madhumuni ya utafiti. Tasnifu hii
imegawanywa katika sura sita. Sura ya kwanza imejumuisha utangulizi. Katika sura
ya pili pana mwauo wa maandishi yanayohusiana na utafiti huu pamoja na misingi ya
kinadharia. Sura ya tatu imeshughulikia mbinu za utafiti zilizotumiwa katika utafiti
huu. Katika sura ya nne na tano, data imechanganuliwa, kuwasilishwa na matokeo
kujadiliwa. Hatimaye, sura ya sita inatoa mahitimisho na mapendekezo kutokana na
utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kuwa ushairi wa Kiswahili ni utanzu
wa fasihi ulio na umuhimu mkubwa katika kuhifadhi matukio mbalimbali ya
kihistoria. Kupitia uhifadhi huu, sifa na vitendo vya mwanasiasa wa Afrika
vimebainika katika vipindi mbalimbali vya kisiasa. Imebainika kuwa mwanasiasa wa
Afrika aliyeonekana kuwa mzalendo kabla ya uhuru alibadilika ghafla uhuru
ulipopatikana na kuwa mkandamizaji wa umma alioapa kulinda. Aidha, wanasiasa
walioonekana kutetea upatikanaji wa demokrasia ya vyama vingi hawajatekeleza
demokrasia hiyo. Licha ya dosari zilizobainishwa na utafiti huu, ni dhahiri kuwa bara
la Afrika bado lina wanasiasa wachache vielelezo ambao wanaweza kuigwa na
wanasiasa wa wakati huu na wale wa baadaye. Matokeo ya utafiti huu yatawanufaisha
wasomi wa Kiswahili, waandishi na washikadau wote wa masuala ya kisiasa barani
Afrika na kwingineko ulimwenguni.