Ubandikaji Majina na Majumlishi Memeto kama Mikakati ya Propaganda Katika Mdahalo wa Urais wa Kenya 2013
Abstract
Wanasiasa hutumia mbinu anuai kuelekeza uelewa wa suala la kisiasa; mikakati ya propaganda
haswa ndiyo hutumika zaidi katika kampeni za kisiasa miongoni mwa wanadamu wote ulimwenguni.
Shida kubwa ni kama jamii ya kistarabu na kibinadamu inaweza kuendelea kuthamini na kushiriki
katika propaganda katika shughuli za uteuzi wa uongozi: kwani kwenye propaganda huwa kupiga
chuku,uongo, chuki na mambo mengi ambayo ni kinyume na kutangamana kwa wanadamu kama
washiriki wenza katika jamii. Kazi hii imetathmini namna mikakati miwili ilitumiwa na wagombea wa
kiti cha urais nchini Kenya, mwaka wa 2013, kwa lengo la kushawishi wapiga kura na kujipa
umaarufu. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Hakiki wa Matini. Data ilikuwa kauli
zilizoingiana na mikakati ya propaganda. Uchanganuzi ulizingatia maarifa ya kithamani, ya
kimaudhui na kiuhakiki. Matokeo yalionyesha matumizi ya ubandikaji majina na majumlishi memeto.
Tekniki hizi zilitumiwa na wagombea kwa lengo la kujijengea sifa njema huku wakilenga kubomoa
sifa za wapinzani. Pia zilitumiwa kwa dhamira ya kuuza sera za vyama vyao huku wakidhamiria
kudhalilisha sera za wapinzani. Kazi hii ni mchango adimu kwa taaluma ya uchanganuzi matini na
mawasiliano ya kisiasa. Aidha ni ya manufaa kwa wanafunzi wa uchanganuzi matini, sayansi ya siasa
na mawasiliano. Tafiti zaidi zinaweza kufanywa kuhusu mbinu nyingine kama vile balagha, na pia
kuzingatia nadharia zingine tofauti zinazohusu uchanganuzi wa matini.